KISWAHILI NA UCHUMI WA KIDIJITALI

KSh0.00

somdn_product_page
Category:

Description

Chapisho hili lenye anwani Kiswahili na Uchumi wa Kidijitali ni zao la makala teule zilizofanyiwa utafiti wa kina na kuwasilishwa katika kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro mnamo Machi 2024. Kongamano hilo liliwaleta pamoja wataalam na wakereketwa wanaohusika na malezi ya lugha adhimu ya Kiswahili kutoka vyuo vikuu na taasisi nyinginezo ulimwenguni. Kongamano hilo lilitoa fursa nzuri kwa wataalam kujadili upekee na uwezo wa lugha ya Kiswahili wa kutumiwa katika kuendeleza uchumi wa kidigitali. Aidha, mabingwa hawa walikongamana ili kudhihirisha namna ambavyo Kiswahili kinatumiwa katika majukwaa mbalimbali ya kidijitali, hivyo kukikuza na kukiwezesha kuwa lugha ya matumizi mapana ulimwenguni. Chapisho hili limegawika katika sura nne ambapo masuala anuwai yanayohusu maendeleo ya elimu, lugha, isimu na fasihi ya Kiswahili katika ulimwengu wa kidijitali yamepambanuliwa kwa utondoti. Mathalani, Sura ya Kwanza imeshughulikia masuala ya Fasihi Andishi katika Enzi ya Kidijitali, huku Sura ya Pili ikiangazia taaluma ya Fasihi Simulizi katika Enzi ya Kidijitali. Kadhalika, Sura ya Tatu imedadavua masuala ya Elimu ya Kiswahili katika Enzi ya Kidijitali. Hatimaye, Sura ya Nne imepambanua namna ambavyo Kiswahili kinatumiwa katika Ujasiriamali, Ubidhaaishaji na Uchumi wa Kidijitali. Kitabu hiki basi kitakuwa hazina aali kwa wasomi na watafiti wa taaluma za Kiswahili.

[Sura za kitabu hiki zimeangazia masuala ainati za taaluma za lugha, isimu, elimu na fasihi kidijitali. Kitabu hiki kinatokea kama hazina muhimu itakayowafaa wasomi na wapenzi wote wa Kiswahili katika ngazi zote za elimu – Prof. Ernest Sangai Mohochi, Chuo Kikuu cha Kibabii, Februari 2025].

Dkt. Fred Simiyu ni mwenyekiti wa CHAKITA na Mhadhiri Mwandamizi wa  fasihi, lugha na utamaduni katika Chuo Kikuu cha Kibabii. Yeye ndiye mwandishi wa Kitovu cha Fasihi Simulizi; Misingi ya Ukalimani na Tafsiri; Stadi za Mawasiliano na Mbinu za Ufundishaji wa Kiswahili; Concise Trilingual English-Kiswahili-French Dictionary; na Safina ya Utafiti katika Fasihi Simulizi.

Prof. Evans Mbuthia ni Profesa Mshiriki katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Mbuthia amebobea katika masuala ya fasihi, hasa hadithi fupi na hadithi za watoto. Amehariri diwani kadhaa za hadithi fupi na kuandika hadithi fupi nyingi na makala kadhaa katika majarida tofauti ya Kiswahili.

Dkt. Mark Odawo ni Mhadhiri  katika Chuo Kikuu  cha Egerton. Odawo ana tajriba pana ya kufunza taaluma za Kiswahili katika ngazi tofauti. Ameandika makala nyingi na kuchangia katika sura ya vitabu kadhaa. Odawo ni mbobezi na mfuatilizi wa masuala ya tafsiri na pragmatiki.

Dkt. Tecla Ngisirei ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Moi. Tecla  amebobea katika masuala ya Isimu. Pia, ameandika makala nyingi katika majarida ya Kiswahili.

Dkt. Deborah Amukowa ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Maseno. Amebobea katika ufunzaji wa fasihi na historia ya maendeleo ya Kiswahili. Ameandika makala nyingi katika majarida mbalimbali ya Kiswahili.

Dkt. Fridah Miruka ni Mhadhiri mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Masinde Muliro. Fridah ni mkuu wa Kitengo cha Kiswahili na mhariri wa Jarida la Kiswahili Sanifu la Chuo Kikuu cha Masinde Muliro. Miruka ameandika makala kadhaa katika majarida tofauti ya Kiswahili.

Reviews

There are no reviews yet.

Be the first to review “KISWAHILI NA UCHUMI WA KIDIJITALI”

Your email address will not be published. Required fields are marked *