Utafiti na Uchanganuzi wa Fasihi Tafsiri ya Kiswahili

Category:

Description

Utafiti na Uchanganuzi wa Fasihi Tafsiri ya Kiswahili ni kitabu kilichoandikwa kutoa ufafanuzi wa kinadharia na kiutekelezi wa dhana, taratibu, mikakati na michakato ya kufanya utafiti wa kifasihi, hususan utafiti wa fasihi tafsiri. Kitabu hiki kinakita kuwili: kwanza kinaangazia kwa ujumla masuala, dhana, michakato na vielelezo vya kiutafiti vinavyoshirikishwa katika utafiti wa kifasihi kwa jumla; pili, kitabu hiki kinaangazia kwa undani utafiti wa fasihi tafsiri ya Kiswahili hasa. Kwa hivyo, kitabu hiki kimezitalii na kuziangazia dhana, fafanuzi, nadharia na mbinu za utekelezaji wa utafiti wa fasihi tafsiri ya Kiswahili. Ni kitabu ambacho kinatoa mitazamo miwili mahususi ya kiuchanganuzi – uchanganuzi changamano wa matini tafsiri za kifasihi kama inavyoakisika katika tafsiri ya Wema Hawajazaliwa, na uchanganuzi wa kipengele mahususi cha usanifu wa kifasihi – tafsiri za methali, semi na misemo kama inavyoonyeshwa kiutekelezi katika tafsiri ya Mshale wa Mungu. Kwa maana hii, ni matumaini yangu kwamba kitabu hiki kitawafaa wahadhiri, wasomi, watafiti na wanafunzi wa vyuo vikuu wanaojishughulisha au wanadhamiria kubobea katika uga huu wa fasihi tafsiri. Hali kadhalika, kitawanufaisha wasomi wanaotafiti kuandika makala za kiusomi zinazoangazia masuala ya fasihi tafsiri. Hata kama hii ni hatua ya mwanzo katika vitabu vinavyokusudiwa kuandikwa katika uga huu, kitabu hiki kitawafaidi wapenzi na wakereketwa wa taaluma hii kwa maana kimekuja katika wakati mwafaka na kitachangia kupunguza kuchanganyikiwa kulioko katika utafiti na uchanganuzi wa fasihi tafsiri.

Zaja J. Omboga ni mhadhiri mwandamizi katika Idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Nairobi. Zaja ana shahada ya uzamifu kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta, na shahada ya Uzamili na ya kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi. Ni mhadhiri, mtafiti na mtafsiri mwenye tajriba pana aliyebobea katika masuala ya nadharia za tafsiri, fasihi tafsiri na tafsiri tekelezi katika taaluma mbalimbali, ni mwandishi wa vitabu, makala katika majarida ya kitaifa na kimataifa pamoja na sura katika vitabu vya kimataifa. Ameshirki katika uandishi wa kamusi, amesimamia na kuwa mshauri katika uandishi wa tasnifu za uzamili (83) na uzamifu (6) licha ya kuwa mtahini katika vyuo vikuu ndani na nje ya nchi.

Reviews

There are no reviews yet.

Be the first to review “Utafiti na Uchanganuzi wa Fasihi Tafsiri ya Kiswahili”

Your email address will not be published. Required fields are marked *