Description
Kitabu hiki kinabainisha namna watunzi wa fasihi hutumia tashtiti kutaja yasiyotajika bila kuchukiza, kuchukuliwa vibaya au kumwudhi msomaji. Tashtiti ni mbinu ya kuweka wazi na kurekebisha uovu na ujinga katika jamii kwa ucheshi. Tashtiti haiibui tu ucheshi bali ni ucheshi wenye lengo la kurekebisha. Nadharia Mfumo Tashtiti ya Highet inafafanua tashtiti kwa vipengele vyake kumi na moja ambavyo ndivyo huunda mfumo wa tashtiti. Vipengele hivi kumi na moja ni; kinaya, ukweli kinzani, mpomoko, tabaini, mwigo wa kubeza, usemi wa kimtaa, pujufu, vurugu, uangavu, chuku na mada za siku. Kitabu kinadhihirisha namna waandishi, kupitia kazi zao za fasihi, hufanyia mzaha mambo mazito wakiwa na lengo la kufichua uovu na ujinga katika jamii kwa ajili ya kuurekebisha. Kitabu hiki ni cha kipekee kwa namna kilivyosanifiwa. Mwandishi amepambanua tashtiti na vipengele vyake kwa njia ya wazi, ya kusisimua pamoja na mifano ya tungo za fasihi ambamo tashtiti imetumika. Utungo huu unapendekezewa wanafunzi wa fasihi katika vyuo vikuu, wahadhiri, watafiti na wadau wote katika elimu ya juu, mno wanataaluma wa Kiswahili.
Dkt. Nancy K. Ayodi alihitimu shahada ya Uzamifu (Chuu Kikuu cha Egerton), Uzamili katika Kiswahili (Chuo Kikuu cha Moi) na Elimu (Chuo Kikuu cha Kenyatta) kwa kujikita katika somo la Kiswahili na Dini. Kwa sasa, yeye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara ambako amewafunza na kuwalea hadi kuhitimu wanafunzi kadhaa wa shahada ya kwanza, wazamili na wazamifu tangu mwaka wa 2009 hadi leo. Amechapisha makala mengi katika majarida na vitabu vya Kiswahili katika uwanja wa Kiswahili, Fasihi na lugha nyinginezo za Kiafrika. Pia, amehudumu katika nyadhfa mbalimbali za uongozi katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara: Kiongozi wa Mitaala ya Kiakademia idarani mwake (2020 hadi sasa); Mkuu wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi Jamii (2018-2020); Mkurugenzi wa Bewa la Nairobi la Maasai Mara (2014-2017). Kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Maasai Mara, alikuwa Mwalimu wa Kiswahili katika vyuo na shule za sekondari nchini Kenya: Chuo cha Tekinolojia na Sayansi cha RVST, Nakuru; Chuo cha Walimu cha Mosoriot, Nandi; shule za upili Moi Kabarak Nakuru; Kilimo, Njoro na shule ya wasichana ya Kapropita, Baringo. Mbali na haya, amehudhuria na kushiriki makongamano na warsha anuwai nchini na nje: Chuo Kikuu cha Kichina cha Hongkong, Hongkong; Chuo Kikuu cha Bayreuth, Ujerumani, Capetown, Afrika Kusini, Chuo cha Juniata, Pennyslavania, Marekani na katika vyuo vikuu vingi katika Jumuiyia ya Afrika Mashariki.
Reviews
There are no reviews yet.